BALOZI ZENA AKUTANA NA PRINCE TURKI BIN SULTAN AL SAUD KUJADILI FURSA ZA BIASHARA
Riyadh, 17 Novemba 2026
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ufalme wa Saudi Arabia, Mhe. Mhandisi Zena Ahmed Said, alikutana na kufanya mazungumzo na Prince Turki bin Sultan Al Saud, Mmiliki wa Kampuni ya Star Technology For Trading, katika Ofisi za Ubalozi mjini Riyadh, tarehe 17 Novemba 2026.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kupanua fursa za bidhaa za Tanzania kuingia katika soko la Saudi Arabia na nchi nyingine za Ghuba. Katika mkutano huo, Prince Turki alieleza nia ya kampuni yake kuagiza bidhaa mbalimbali kutoka Tanzania, hususan mafuta ya kula, mazao ya kilimo na bidhaa za chakula.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi alieleza utayari wa Ubalozi kushirikiana na taasisi husika nchini Tanzania katika kuwaunganisha wafanyabiashara hao na wazalishaji pamoja na wasambazaji wa bidhaa zinazohitajika. Aidha, pande hizo zilijadili uwezekano wa ujumbe wa kampuni hiyo kufanya ziara ya kibiashara nchini Tanzania ili kujionea fursa zilizopo na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na wadau wa biashara.
Pichani: Mhe. Balozi Zena Ahmed Said akiwa na Prince Turki bin Sultan Al Saud mara baada ya mkutano huo uliofanyika Ubalozini Riyadh.

