Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhandisi Zena Ahmed Said, ameshiriki uzinduzi wa filamu maalum inayohusu masuala ya utalii na mazingira iitwayo ‘Seven Summits’ uliofanyika jijini Riyadh. Filamu hiyo, iliyoandaliwa na taasisi ya Cinerama Film Club, inaonesha safari ya mpanda milima mashuhuri wa nchi hiyo, Dkt. Badr Al Shibani, ambapo alitimiza azma yake ya kupanda kilele kimoja kirefu zaidi katika kila bara duniani, ukiwemo Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Dkt. Badr alieleza kuvutiwa kwake kipekee na Mlima Kilimanjaro huku akiwahimiza watu kuitembelea Afrika, Kwa Kuanzia Mlima Kilimanjaro. “Napanga kurudi tena nchini Tanzania nikiwa na familia yangu kwa ajili ya kupanda mlima Kilimanjaro, pamoja na kutembelea hifadhi za Serengeti na Ngorongoro” alisema Dkt. Badr.
Kwa upande wake, Balozi Zena alimpongeza Dkt. Badr kwa ujasiri mkubwa uliomwezesha kuingia kwenye historia ya kuwa miongoni mwa watu wasiozidi 600 duniani kote waliokamilisha ‘Seven Summits Challenge’. Alifafanua kuwa filamu hiyo imekuwa chombo muhimu cha kuitangaza sekta ya utalii ya Tanzania kimataifa kupitia picha na maelezo ya mlima huo mrefu zaidi barani Afrika. Alitumia fursa hiyo kuwahamasisha raia wa Saudi Arabia na wageni wengine kutembelea vivutio vya kipekee vilivyopo nchini.


