Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhe. Mhandisi Zena Ahmed Said, amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Mabalozi nchini humo, Mhe. Dkt. Dya-Eddine Said Bamakhrama, jijini Riyadh. Lengo la mazungumzo hayo ni kujitambulisha, kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa Diplomasia ya uchumi na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao nchini Saudi Arabia.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Bamakhrama alieleza kuwa Saudi Arabia inaendelea kuwa mhimili muhimu wa diplomasia ya kimataifa na mji wa Riyadh ni miongoni mwa miji salama na rafiki kwa uwekezaji. Aidha, alieleza uzoefu wake kuhusu mikakati bora ya kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa ufanisi ili kuleta manufaa kwa mataifa yanayowakilishwa. Dkt. Bamakhrama pia alipongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia, huku akimkaribisha rasmi Balozi Zena katika jumuiya ya wanadiplomasia nchini humo. Alimtakia mafanikio katika kutekeleza majukumu yake ya uwakilishi na kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Balozi Zena alisema Tanzania na Saudi Arabia zimejenga ushirikiano wa muda mrefu wenye manufaa kwa pande zote mbili. Alisisitiza kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano huo, hususan katika nyanja za biashara, uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi. Aliahidi kuendeleza ushirikiano na Jumuiya ya wanadiplomasia nchini Saudi Arabia huku akimkaribisha Dkt. Bamakhrama kutembelea Tanzania na kumkabidhi zawadi ya picha maalum inayoonesha baadhi ya vivutio vya utalii vya Tanzania, kama ishara ya urafiki na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.